Showing 1–20 of 37 results

Dhulma na Abdulrazak Gurnah

KShs2,200.00
Katika mitaa ya Zanzibar na Dar es Salaam, maisha ya vijana watatu–Badar, Karim, na Fauzia–yanasukwa na matukio yasiyotabirika. Badar, kijana maskini asiye na mizizi wala elimu, anajikuta katika dunia ya watu wenye mamlaka na mali. Akiwa mtumishi, bahati inampiga mawimbi anapokutana na Karim–kijana wa mama mwenye nyumba, mwenye ndoto na matarajio makubwa. Wakati huo huo, Fauzia, bado akiwa kaelemewa na changamoto za utotoni, anatafuta njia ya kujinasua. Vijana hawa wenye njozi tofauti lakini mustakabali uliofungamana, wanapita kwenye safari ya mapenzi, kazi na uzazi, huku urafiki wao ukijaribiwa na tamaa, hofu, mabadiliko ya kiuchumi na teknolojia na hatimaye–usaliti. Je, hatima yetu huamuliwa na hadhi ya kuzaliwa kwetu, au tunaweza kuiandika upya? Hakika simulizi hii inatupeleka kwenye safari ya maisha ya wale wanaotafuta nafasi yao katika ulimwengu unaobadilika haraka, usio na huruma na wenye dhulma bila kujali walipotoka. Hii ni Tafsiri ya Riwaya ya Kwanza ya Abdulrazak Gurnah baada ya kutunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi ya mwaka 2021.

Safari ya Mauti

KShs1,300.00 KShs1,000.00
Insi awapo katika himaya yake ya kuendeleza ghorofa ya maisha, katu huwa katika baraste iliyojaa mengi asiyoyajua. Je, umewahi kujikuta kwenye njia usioijua? Kulingana na wasomi ni wazi kuwa kupotea njia ndiko kujua njia. Riwaya hii itakupa jibu mwafaka! Safari ya Mauti imemsawiri binadamu katika ubinadamu wake wa sura, maumbile na hisia. Maudhui mengi ya kisasa yamechorwa ili kumpa msomi namna ya kuzikabili hali katika harakati zake za kila leo. Mathalani; Elimu, Ufisadi, Siasa, Dini, Tandavu, Teknolojia na Mapenzi ni miongoni mwa maudhui ainati yaliyokiumba kitabu hiki chenye mnato. Umilisi wenye mwonjo wa fani kochokocho za lugha umeipamba na kuiremba riwaya hii. Mwandishi Bw. Gitonga amekuandalia fasihi yenye utamu na wingi wa tafiti. Usikose kukiwahi katika maduka ya vitabu. Ama kweli aendaye kisimani mbele hunywa maji maenge.

Roho ya Paka by Ben Mtobwa

KShs990.00
Inspekta Kombora anaitwa katika hoteli moja jijini Dar es Salaam ambapo anaonyeshwa mwili wa msichana aliyeuawa kikatili kupita kiasi. Ngozi na nyama ya uso wake mzima na sehemu ya shingo zimeliwa na aina fulani ya sumu na kufanya sura yake ibakie kuwa fuvu la kutisha. Katika kinywa cha fuvu hilo, uliwekwa ujumbe kwa maandishi uliosomeka: Tunamtaka Joram Kiango. Salamu zinamfikia Joram kwa namna nyingine. zikifuatiwa na patashika nzito, roho mkononi, huku watu wengi walio na wasio na hatia wakipoteza roho zao. Lakini ni roho ya Joram Kiango iliyohitajika, kwa udi na uvumba. Naye, akijua kuwa anapambana na mbogo waliojeruhiwa, alichukua tahadhari zote kutopoteza uhai mithili ya paka. Hata roho yake pia inabadilika na kuwa Roho ya Paka.

Mikataba Ya Kishetani by Ben Mtobwa

KShs790.00
Alielezwa kuwa mlengwa wake atakuwa amevaa suruali nyeusi ya kitambaa, yenye rangi nyeusi na koti la rangi ileile, juu ya shati lenye rangi ya bendera ya taifa. Atatoka nje ya mlango wa hoteli saa nne na robo, akiwa katikati. Rais wa nchi kulia kwake na mgeni wake, bilionea wa viwanda na machimbo ya madini, upande wa pili. Pale mlangoni watasita kidogo kuagana, kabla ya kuelekea kwenye hafla maalumu. Akatakiwa ammalize akiwa palepale mlangoni. Nani mwajiri wake aliyeidhinisha kifo cha msichana huyo mpole, asiye na madhara? Ni nani mkatili huyu, na liwezaje kuwa na hakika ya muda na mavazi atakayovaa siku ya kifo chake!?

Kiguu na Njia by Ben Mtobwa

KShs990.00
Akiwa bado kijana mdogo, Mtukwao anatoroshwa kijijini na familia yake ili aokoe uhai wake ulio katika hatihati ya kupotelea mikononi mwa wanakijiji. Safari inamjia ghafla kama jinamizi na kumfungulia dunia mpya yenye chungu na tamu lakini chungu ni zaidi. Ni pale anapokumbuka kitu muhimu sana alichokipoteza wakati wa pilika zake za maisha, ndipo anapopata wazo la kurudi kwao ili akatengeneze mambo yake. Lakini imekwishapita miaka zaidi ya thelathini tangu aondoke kijijini. Je, familia yake ambayo ndiyo ina dhamana pekee ya kumsaidia, bado ipo? Ama ndiyo ng’ombe wa maskini hazai? Katika kitabu chake hiki cha mwisho, Ben R Mtobwa anathibitisha kwa mara nyingine uwezo wake mkubwa wa kuitumia kalamu yake bila kubahatisha. Kinachotofautisha riwaya hii na riwaya nyingine za Ben Mtobwa, ni namna mwandishi huyo alivyohama kabisa kutoka kwenye maudhui ya kijasusi na kuchambua uhalisia wa watanzania wengi. Kutana na mhusika aliyetembea karibu kila mkoa, akionesha ama kwa maneno ama kwa matendo, uchumi, jiografia, historia pamoja na mila na desturi za eneo husika.

Siku Saba za mwendawazimu by Felistas...

KShs1,090.00
SIKU SABA ZA MWENDAWAZIMU ni riwaya iliyosheheni visa mbalimbali vinavyoelezea matatizo yanayojitokeza katika jamii. Katika riwaya hii ya kusisimua, mwandishi anawachora Kikopo na Mfuniko kama wahusika wendawazimu lakini katika hali yao ya uendawazimu, wahusika hawa wakuu pamoja na wahusika wengine wanaonesha ni changamoto zipi wananchi, hasa wa kipato cha chini, wanakabiliana nazo. Mwandishi anazungumzia pia suala la thamani ya maadili na umuhimu wa kujitambua, kukubali na kudumisha utamaduni wetu. Hii ni hadithi iliyojaa kejeli na ucheshi ndani yake. Mwandishi anatumia mbinu hii ya kejeli na ucheshi kuwasilisha ujumbe muhimu kwa jamii.

Maji Hayafuati Mkondo by Felistas Mah...

KShs890.00
MAJI HAYAFUATI MIKONDO ni riwaya ya kipekee iliyoandikwa na mwandishi wa kike Felistas Richard Mahonge. Riwaya hii inazungumzia changamoto anazokumbana na mwanamke katika kufikia ndoto za maisha yake. Mama Sinta, Sinta na Mercy ni wahusika ambao mwandishi anawatumia katika kuonesha mchango wa mwanamke katika kujenga familia kimaadili na kiuchumi. Wahusika hawa wanachorwa na mwandishi kama wanawake wenye utashi mkubwa wa kupambanua mambo pamoja na ujasiri mkubwa katika kupambans na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yao. Kwa kutumia wahusika hawa na wengine, mwandishi anasisitiza suala la umuhimu wa wazazi kushiriki kwa pamoja katika kulea watoto na kuijenga familia kwani ndio mhimili wa taifa lenye uadilifu. Mwandishi anapiga vita wazazi na walezi ambao wanashiriki kwa makusudi katika kuangamiza kizazi kipya Anakemea suala la matumizi ya madawa ya kulevya, biashara ya binadamu pamoja na rushwa. Mwandishi anaonesha pia umuhimu wa vyombo vya dola katika kusimamia haki za wanaodhulumiwa katika jamii.

Mdunguaji by Hussein Issa

KShs1,050.00
Wapiganaji kumi, wakiwemo Watanzania watatu, wanaounda kikosi maalum cha jeshi la Umoja wa Mataifa kilichotumwa kulinda amani nchini Sierra Leone, wanashambuliwa na mdunguaji aliyejificha katika msitu walikokuwamo. Sita kati yao wanauawa, mmoja baada ya mwingine, kwa kudunguliwa na mdunguaji huyo hatari. Ni Mtanzania mmoja tu ndiye anayerudi nchini akiwa hai, huku akirejesha nyumbani miili ya wapiganaji wawili waliouawa na mdunguaji huko Sierra Leone, Miaka mitatu baadaye, mpiganaji aliyeshinda vita vingi vya msituni, Baddi Gobbos, anajikuta akikabiliana na vita vingine katikati ya jiji la Dar pale anapojikuta akiwindwa na wauaji asiowajua. Je, mdunguaji wa Sierra Leone kaingia Tanzania? Wakati huo huo Baddi Gobbos anajikuta akiwa mateka aliyeshindwa katika vita vigumu kuliko vyote alivyowahi kukabiliana navyo maishani mwake... vita vya mapenzi...

Takadini by Ben Hanson

KShs590.00
Riwaya ya kipekee inayovuta hisia, ambayo inasawiri mila na desturi huku ikijikita katika karne ya 19 nchini Zimbabwe. Japokuwa ilikuwa ni mwiko kuruhusu kuwepo kwa mazeruzeru, yaani wakipokonywa maisha yao punde wazaliwapo, mwanamke mmoja jasiri anamtoroshaTakadini, mwanawe aliye zeruzeru ili kuyanusuru maisha yake.
 
Lakini, hata katika nchi wanayokimbilia, jamii inavutana sana, wengi wakiamini kuwa kuwepo kwa Takadini na mama yake kungewaletea mkosi. Hata hivyo, baadhi ya wazee wanatumia busara kuupoza mgogoro huo, japokuwa kwa vikwazo vingi.
 
Takadini, alikuwa sope yaani zeruzeru na hatimaye alipata ulemavu, akatengwa na watoto wenzake huku wengine wakimkejeli. Katikati ya unyonge na mashaka, Takadini na mama yake wanafarijika kwa mapenzi wanayopewa na Baba Chivero, mganga mashuhuri ambaye kabla hajafa anamfundisha Takadini tiba mbalimbali. Hata Takadini anapoibuka kuwa mpigaji mbira hodari, hatimaye jamii inaanza kuvutiwa naye. Akatokea msichana akampenda, wakaoana na wakapata mtoto asiye sope. Kumbe, ulemavu wake na uzeruzeru wake, havikumzuia kuyatenda yale wafanyayo binadamu wengine.

Uchororo wa Tanzanite by Wilbard Makene

KShs990.00
Alex, afisa usalama, anapenyezwa Wizara ya Madini kufichua kinachoendelea katika upotevu tata wa mapato ya Taifa ndani ya biashara ya madini ya Tanzanite. Anaambulia taarifa kiduchu.
 
Kitendawili kinabaki, ni kina nani wanahusika na biashara hii haramu kimataifa?
 
Kutegua kitendawili, Alex anaondolewa wizarani na kutumwa kwenye misheni ya siri. Lengo ni kufichua mtandao ili hatimaye Taifa lipate kuudhibiti Uchochoro mzima wa Tanzanite. Alex anakutana na mauaji, usaliti, visasi na ukatili kutoka kwa magenge ya wahalifu ya kimataifa.

Maji Mandiga by Mohammed Hammie

KShs690.00
Maji ni mhimili wa maisha. Si rahisi kutambua hili kwa kina na mapana stahiki katika maisha ambayo maji yanapatikana. Katika kisa hiki, mwandishi anatufungulia dirisha la kuona msururu wa tabu na visa vya kusikitisha anavyokumbana navyo mwanamke. Hili linatokea kwa kuwa anayatafuta maji penye uhaba mkubwa, mazingira duni na kukithiri kwa mila na desturi kandamizi. Kutana na mwanamke, Mandiga, upate kufahamu maisha ambayo mwanamke katika kijiji duni cha Kiafrika anapitia.

Gamba la Nyoka by Euphrase Kezilahabi

KShs890.00
Gamba la Nyoka ni riwaya inayosawiri mapambano kati ya dola na wananchi wa hali ya chini waliogomea utekelezaji wa mifumo ya uzalishaji mali iliyowalazimisha kuondoka katika maisha na maeneo waliyoyafahamu baada ya ukombozi. Mwandishi anaangazia namna dola ilivyotumia mabavu kupambana na wakulima wa kawaida ambao hawakukubaliana na uamuzi wa kuwahamisha kutoka katika makazi yao ya jadi na kuwapeleka katika vijiji "vilivyopangwa." Ni riwaya inayoangazia pupa za kisiasa katika kufanya uamuzi, na athari zake kwa watu wa kawaida. Unjozi wa mawanio ya kujenga mfumo mpya vijijini unaoneshwa, na hali kadhalika vikoa vya upinzani, baadhi vikiwa ndani ya makanisa na baadhi ndani ya serikali yenyewe. Mbali na uhalisia huo, riwaya inaeleza pia falsafa ya mwandishi kuhusu maisha na ubaho, kuhusu dini, imani na Mungu, na kuhusu mabadiliko na mageuzi duniani.

Mzingile by Euphrase Kezilahabi

KShs690.00
Mzingile ni novela (riwaya fupi) ya kifalsafa na kibaadausasa iliyochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1991. Riwaya hii ni pacha ya ile ya Nagona (1990). Riwaya hii inasawiri chimbuko, maendeleo, maangamizi na kuzaliwa upya kwa dunia kutokana na fujo za wanadamu.
 
Kakulu, mhusika kiini wa novela hii, anasemekana kuwa alizaliwa kiajabuajabu, na umbo lake na maisha yake kwa jumla yalikuwa ni ya kushangaza na kutatanisha, yakihusishwa na matukio ya ajabu na uwezo usio wa kawaida aliosadikiwa kuwa nao. Hatimaye Kakulu anajitenga na jamii na kwenda kuishi peke yake juu ya kilima, lakini watu hawamwachi kwa amani kama anavyotaka, bali wanaendelea kumfuata na kumsujudia na kumhusisha na mambo ambayo yeye anasema hahusiki nayo. Hata baada ya karne nyingi bado watu wanamwamini na kumsujudia. Kwa njia hii kisasili cha Kakulu kinaundwa na uvumi unageuka kuwa ukweli. Unapotokea msiba unaodhaniwa kumhusu, anatumwa mjumbe (Msimulizi) kwenda kumtafuta Kakulu kumwarifu juu ya msiba huo. Safari hiyo ya karne nyingi inageuka kuwa msako wa utambuzi na ufunuo, na kuishia katika amagedoni inayoifuta dunia kongwe na kuasisi dunia mpya iliyo nje ya duara la Kakulu.
 
Hii ni hadithi ya kifalsafa inayosaili simulizi kuu zinazotawala duniani, ikiwamo ile ya kuumbwa, kuanguka na kukombolewa kwa dunia. Riwaya hii inatuchochea kuyatazama kwa jicho jipya yale tuliyozoea kuyafikiria kuwa kweli isiyosailika, zikiwamo imani za dini, siasa na sayansi. Ni hadithi inayoifikisha riwaya ya Kiswahili katika kiwango cha juu cha tafakuri na sanaa. Inafaa kusomwa na kila binadamu anayejali asili na hatima ya ulimwengu huu na watu wake.

Kichwamaji by Euphrase Kezilahabi

KShs890.00
Kichwamaji ni riwaya inayosawiri tabaka la vibwanyenye wasomi na warasimu, ambao elimu yao ya kimagharibi imewapumbaza na kuwakengeusha, hivyo kuwa mbali na jamii zao. Elimu hii inakuwa ni chanzo cha mgogoro mkubwa baina ya kizazi cha vijana na kizazi cha wazee. Matokeo ya ukengeufu huu ni kuangamia si tu kwa vijana wenyewe bali hata kizazi chao.

Simu ya Kifo by Faraji Katalambulla

KShs690.00
Mzee Jacob anafariki ghafla akiwa nyumbani kwake. Uchunguzi unabajnisha kuwa amefariki kwa kuvuta sigara yenye sumu. Siku chache baadaye, binti yake, Mary anapigwa risasi. Msururu wa vifo unaendelea kutokea mbali ya kuwa inspekta Wingo anajitahidi kufuatilia kwa karibu kuweza kubaini chanzo na mhusika wa mauaji haya. Mbaya zaidi, kila kifo kinapotokea, FAMBO anampigia inspekta Wingo simu na kumtaarifu kuwa punde si punde fulani atafariki. Je, inspekta Wingo anaweza kutegua kitendawili na kuzuia kifo kinachotazamiwa kutokea? Na je, FAMBO ni nani hadi afahamu yajayo? Na je, anahusika katika mauaji haya?

Sarafu ya Gavana by Wilbard Makene

KShs790.00
Watu wasiojulikana katika nchi ya Weusi Kusini, wanapambana vikali kumshambulia Gavana wa nchi hiyo, bwana Bongo kwa lengo la kummaliza. Katika hali ya kushangaza, vyombo vya usalama vya nchi ya Weusi Kusini, ambavyo vilipaswa kumpa ulinzi Gavana, vinasuasua kufanya hivyo. Hofu na mashaka vinatamalaki kichwani mwa Gavana; mnyororo wa maswali unajirefusha kichwani mwake. Ndipo anapoibuka Elvis Madiba, kijana machachari kutoka ndani ya vyombo vya usalama. Anamfuata Gavana na kumwachia sarafu. Huo ndiyo unakuwa mwanzo wa kuibuka chuki na uhasama, visasi na uhalifu, minyukano, nk

Wimbo wa Gaidi by Hussein Issa Tuwa

KShs1,050.00
Brey Jabba anarudi Tanzania akiwa na fedha nyingi baada ya kukamilisha jukumu kubwa na la hatari sana nje ya nchi; na kulazimika kwenda kuishi kijijini - mbali na jiji kubwa, mbali na watu ambao wangeweza kumtambua, ili akaanze maisha mapya, yenye amani, japo ya upweke.
 
Lakini pale mwanadada kichaa achezaye dansi hovyo mitaani anapomtambua hukohuko kijijini na kumwita kwa jina ambalo hata yeye mwenyewe halitambui, shetani aliyejificha ndani yake anajitokeza, Brey Jabba anaapa kumwangamiza yule "Crazy Dancer". Kisa kinachukua sura mpya pale mtu aliyeweza kuua wauaji waliokubuhu kwa wepesi wa kucheza dansi, anapopata kigugumizi kwenye kumwangamiza yule mwanadada dhaifu mwenye kichaa.
 
Kulikoni?
 
Kama hilo halitoshi, wanapoibuka watu ambao hakutaka kabisa kukutana nao maishani na kumshinikiza ajitokeze kutoka mafichoni, malango yote ya jahanamu yanaonekana kufunguka kinyume naye na kujikuta akiwindwa na wauaji hatari wa kimataifa huku akifuatiliwa kwa karibu na wanausalama wa taifa, ilhali akiandamwa na jinamizi la huba iliyosahaulika.

Joka la Mdimu by Abdallah Saffari

KShs590.00
Riwaya hii inasawiri kisa cha mvuta kwama aliyepora benki ili kumpeleka mwanaye kutibiwa ulaya.